Matthew 4

1Kisha Yesu aliongozwa na Roho mpaka jangwani ili ajaribiwe na ibilisi. 2Alipokuwa amefunga kwa siku arobaini mchana na usiku alipata njaa. 3Mjarabu akaja na akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mkate.” 4Lakini Yesu alimjibu na kumwambia, “Imeandikwa, ‘Mtu hataishi kwa mkate peke yake, bali kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.‘‘’

5Kisha ibilisi akampeleka katika mji mtakatifu na kumweka mahali pa juu sana pa jengo la hekalu, 6na kumwambia,‘’ kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe chini, kwa maana imeandikwa, ‘Ataamuru malaika wake waje wakudake,’ na, ‘watakuinua kwa mikono yao, ili usijikwae mguu wako katika jiwe.”

7Yesu akamwambia, ‘’Tena imeandikwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.‘‘’ 8Kisha, ibilisi akamchukua na kumpeleka sehemu ya juu zaidi akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari ya hizo zote. 9Akamwambia, “Nitakupa vitu vyote hivi ukunisujudia na kuniabudu.”

10Kisha Yesu akamwambia, “Nenda zako utoke hapa, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Yakupasa kumwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’” 11Kisha ibilisi akamwacha, na tazama, malaika wakaja wakamtumikia.

12Basi Yesu aliposikia kuwa Yohana amekamatwa, aliondoka mpaka Galilaya. 13Aliondoka Nazareti alienda na kuishi Kaperanaumu, iliyoko kandokando na Bahari ya Galilaya, mipakani mwa majimbo ya Zabuloni na Naftali.

14Hii ilitokea kutimiza kile kilichonenwa na nabii Isaya, 15“Katika mji wa Zabuloni na mji wa Naftali, kuelekea Baharini, ng’ambo ya Yorodani, Galilaya ya wamataifa! 16Watu walio kaa gizani wameuona mwanga mkuu, na wale waliokuwa wameketi katika maeneo na kivuli cha mauti, juu yao nuru imewaangazia.‘’

17Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri na kusema, “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.‘’

18Alipokuwa akitembea kandokando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aliyekuwa akiitwa Petro, na Andrea kaka yake, wakitega nyavu baharini, kwa kuwa walikuwa wavuvi wa samaki. 19Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate, nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” 20Mara moja waliziacha nyavu na walimfuata.

21Na Yesu alipokuwa akiendelea kutoka hapo aliwaona ndugu wawili wengine, Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana kaka yake. Walikuwa katika mtumbwi pamoja na Zebedayo baba yao wakishona nyavu zao. Akawaita, 22na mara moja wakaacha mtumbwi na baba yao nao wakamfuata.

23Yesu alienda karibia Galilaya yote, akifundisha katika Masinagogi yao, akihubiri injili ya ufalme, na akiponya kila aina ya maradhi na magonjwa miongoni mwa watu. 24Habari zake zilienea Siria yote, na watu wakawaleta kwake wale wote waliokuwa wakiugua, wakiwa na maradhi mbalimbali na maumivu, waliokuwa na mapepo, na wenye kifafa na waliopooza. Yesu aliwaponya. Umati mkubwa wa watu ulimfuata kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu na Uyahuda na kutoka ng’ambo ya Yorodani.

25

Copyright information for SwaULB